Habari

Wakili shauri la ndugu wanaovutana kuhusu mirathi ya Zena ajitoa

SAKATA la ndugu wanaovutana kwenye mirathi ya Zena Jalakhan limechukua sura mpya baada ya Wakili Edward Malando aliyekuwa akimwakilisha Salma Mohammed kwenye shauri hilo kujitoa kwa madai kwamba kuna mgongano wa maslahi.

Taarifa ya kujitoa kwa wakili huyo imewasilishwa leo katika Mahakama ya Mwanzo Nzega mbele ya Hakimu Mfawidhi, Abunas Sonyo.

Wakili Malando aliwasilisha maombi ya kujitoa na kukubaliwa maombi yake lakini Februari 20 mwaka huu akimwakilisha mteja wake aliomba mahakama impe muda aweze kupitia jalada la shauri hilo ili leo amwakilishe mteja wake badala yake amejitoa kwa madai kwamba kuna mgongano wa maslahi.

Wakati shauri linaitwa mahakamani Salma aliwakilishwa na Wakili mwingine ambaye ni Kaumuliza David ambaye aliiambia mahakama kwamba aliajiriwa jana kwa ajili ya kumwakilisha mteja huyo.

Wakili Kaumuliza naye aliomba apewe muda wa kupitia jalada la shauri hilo la mirathi, Mahakama ilikubali maombi hayo.

Upande wa pili wa ndugu hao Karim Samji nao waliomba kuweka mwakilishi, Mahakama ilikubali na kuahirisha shauri hadi Machi 11 mwaka huu.

Shauri hilo lilikuwa mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi lililowasilishwa Februari 13 mwaka huu na Wakili Malando ambaye tayari amejitoa.

Shauri hilo lenye mvutano, upande wa pili wanapinga Karim Samji aliyeteuliwa na Mahakama kusimamia mirathi ya Zena kutekeleza amri ya Mahakama ya kukusanya mali za marehemu.

Salma Mohammed alifungua shauri la mirathi ya Zainabu Jalakhan kwa mali ambayo ni nyumba iliyopo pia katika mirathi ya Zena Jalakhan ambayo mahakama ilishamteua Karim kuwa msimamizi.

Salma aliwasilisha hoja tatu, akidai kwamba shauri linalomuhusu marehemu lilikwisha sikilizwa na kutolewa uamuzi katika shauri la mirathi namba 24/2023.

Hoja ya pili mali iliyotajwa katika maombi hayo ilikwishaorodheshwa katika mirathi namba 24/2023 mbele ya Hakimu Hilda Kibona.

Na hoja ya mwisho ni kwamba shauri hilo lenye viini hivyo lilishasikilizwa na kuamuliwa na mahakama hiyo hivyo aliomba maombi ya mirathi namba 35 ya mwaka jana ya mali ya Zena Jalakhan ambayo mahakama ilimteua Karim kuwa msimamizi yatupiliwe mbali.

Awali Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Sonyo ilimteua Karim kuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya marehemu Zena ambayo ni nyumba iliyopo Mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega mkoani Tabora yenye namba NTC/NMSH/NTI/81..

Mahakama hiyo pia mbele ya Hakimu Hilda Kibona ilimteua Salma Mohammed kuwa msimamizi wa mirathi ya Zainabu Jalakhan ambayo nyumba iliyopo kwenye mirathi ni hiyo hiyo iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.

Hivi karibuni baada ya Mahakama kufanya Usuluhishi kwa familia hiyo, iliamuru aliyeteuliwa kusimamia mirathi, Karim akusanye mali za marehemu.

Hata hivyo katika nyaraka mbalimbali za nyumba hizo ikiwemo risiti za Kodi ya pango iliyowasilishwa mahakamani zinasomeka kwa jina la Zena Jalakhan na si Zainabu Jalakhan.

Karim katika kiapo chake mahakamani alidai marehemu hakuacha wosia na maelezo hayo yaliungwa mkono na wajukuu, Gullam Siager na Haji Seager hivyo mahakama ikamteua kusimamia mirathi hiyo.

Marehemu aliacha nyumba moja iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.

Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Azaz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents